Mwanamuziki Akothee ametilia shaka utendakazi wa ubalozi wa Kenya nchini Saudia Arabia kufuatia kuongezeka kwa visa vya wakenya kudhulumiwa na waajiri wao kwenye taifa hilo la bara Asia.
Akothee ametoa changamoto kwa serikali ya kenya kuchukua hatua madhubuti kuwaokoa wananchi wake kwa utumwa wanaofanyiwa nchini Saudia, akisema mawakala waliotwikwa jukumu la kuwalinda wakenya dhidi manyanyaso hawafanyi kazi yao ipasavyo.
Mwimbaji huyo amesema ni kitendo cha aibu kwa nchi ya kenya kuona wananchi wake wakiteseka ughaibuni wakiwa kwenye harakati za kusaka riziki ambapo ametaka kubuniwe kwa sheria ya kuwazuia watu kusafiri kwenda kufanya kazi nchini Saudia Arabia
Hata hivyo ametoa wito kwa mashariki ya kibinadamu kujitokeza na kushinikiza mabadiliko huku akiwaonya wanawake wa Kenya kuchukua tahadhari kabla ya kusafiri nchini Saudia Arabia kutokana na kuongezeka kwa dhuluma dhidi ya wafanyikazi wa nyumbani.
Kauli yake imekuja siku chache baada ya serikali kumuokoa Diana Chepkemoi na wasichana wengine 20 waliokuwa wamekwama nchini Saudia Arabia.