You are currently viewing Aslay akiri kukataa lebo tatu za muziki kabla ya kujiunga na RockStar

Aslay akiri kukataa lebo tatu za muziki kabla ya kujiunga na RockStar

Mwimbaji wa Bongofleva, Aslay amesema alilazimika kuzikataa Lebo tatu kubwa zilizotaka kufanya kazi na yeye baada ya kuachana na Yamoto Band na kuanza kupata mafanikio kimuziki akiwa pekee yake (solo) kufuatia kuachia ngoma mfululizo.

Katika documentary yake iliyoipa jina ‘Mimi ni Bongo Fleva’, Aslay amesema suala la mikataba na Lebo hizo ndilo hasa lilimfanya kuachana na dili hizo kwa kipindi hicho.

“Kila mtu alikuwa anataka kufanya kazi na mimi, na kikubwa zaidi Lebo kubwa tatu zilinifuata ili kufanya nao kazi, siwezi kuzitaja ila kila moja ilikuja kwa njia yake jinsi inavyotaka kufanya kazi na mimi” amesema.

“Lebo ya kwanza ilikuja, walivyonielezea sikupendezewa na mikataba yao, jinsi wanavyotaka, kwa sababu mimi ni mtu ambaye napenda sana kujiamini, yaani mtu fulani wa kujitoa, kwa hiyo sipendi sana kubanwa kwenye kazi zangu, hivyo nilishindwa kusaini” amesema Aslay.

Amesema Lebo ya pili alisoma mikataba yao lakini akaona haiwezi kumfikisha pale ambapo anataka, hivyo akaamua kuendelea kufanya kazi mwenyewe akiamini ataendelea kufanikiwa kama alivyoanza kwa mafanikio.

Aslay alikuwa miongoni mwa wasanii wanne waliounda kundi la Yamoto Band lilovunjika rasmi mwishoni mwa mwaka 2016, wengine ni Mbosso, Enock Bella na Beka Flavour.

Baada ya kuachana na Yamoto Band, Aslay aliweza kutoa nyimbo 15 ndani ya miezi 11 (Aprili 10, 2017 hadi Februari 22, 2018) na kupata mapokezi makubwa, na hapo ndipo baadhi ya Lebo kutaka kufanya naye kazi.

Utakumbuka hivi sasa Aslay anafanya kazi na RockStar Africa na Sony Music Entertainment Africa ambayo amesaini nayo hivi karibuni, Novemba 18 huko Johannesburg, Afrika Kusini. Aslay ameungana na Ommy Dimpoz, Abigail Chams na Young Lunya ambao wanafanya kazi na Lebo hizo upande wa Tanzania.

Elim Robert

Robert Elim is an Editor with high interest and knowledge in the entertainment space, an industry he has been actively part of since childhood. Leads to breaking stories are welcome at elimrobert@gmail.com & contact@urbanspice.co.ke