Wakati walimwengu wanaendelea kumkosoa Bebe Cool mtandaoni kwa kuachia wimbo wake wa Amapiano uitwao “Nyege Nyege”, msanii huyo ameripotiwa kulipwa takriban shillingi laki 6 za Kenya.
Kulingana na chanzo cha karibu na bosi huyo wa Gagamel, waandaji wa tamasha la Nyege Nyege walimlipa kiasi hicho cha fedha kwa kutunga wimbo huo uliokuwa unasifia tamasha hilo la siku nne linaloendelea kwa sasa huko Jinja nchini Uganda.
“Alilipwa shillingi millioni 20 za Uganda kwa kutoa wimbo huo, hivyo hajali na hatishiki kabisa na maneno ya watu wanaomsema vibaya mtandaoni”, Chanzo hicho kimeiambia jarida moja la Habari nchini Uganda.
Utakumbuka baada ya Bebe Cool kuachia wimbo wa Nyege Nyege alipata ukosoaji mkubwa kutoka kwa mashabiki na baadhi ya wasanii akiwemo Mr. Lee wa B2C na King Saha ambao walihoji kuwa wimbo huo hauna ubora wowote.
Mapema wiki iliyopita tamasha la Nyege Nyege lilisitishwa kwa muda na bunge la Uganda kwa misingi ya kueneza uesharati lakini Waziri mkuu nchini Uganda Robinah Nabanjja alikuja akatengua uamuzi huo wa bunge na kuruhusu tamasha hilo kuendelea.