Mwimbaji wa nyimbo za injili nchini Ben Githae ameonekana kuchukizwa na kitendo cha mashabiki kuendelea kumkejeli hata baada ya mrengo wa azimio la umoja kupoteza uchaguzi mkuu uliokamilika.
Akizungumza kwenye hafla ya kuchangisha pesa huko Mlima Kenya, Githae amekiri kuumizwa sana na kauli ya watu wanaokumbusha kila mara namna mrengo aliokuwa anaunga mkono wa Azimio la umoja ulivyopoteza uchaguzi wa Agosti 9 huku akiwataka marafiki zake kumkubali kama mmoja wao badala ya kumsema vibaya kwa misingi ya kisiasa.
Hitmaker huyo wa “Mabataro” amesema kwa sasa ameshakubali matukio kuwa muungano wa Azimio la umoja ulipoteza uchaguzi huku akisisitiza kuwa hana budi kukumbatia serikali ya Kenya Kwanza inayoongozwa na Rais William Ruto.
Miezi mitano iliyopita Ben Githae alikuwa gumzo nchini baada ya kuachia wimbo wa kisiasa uitwao “Kenya Is Safe”, wimbo ambao alikuwa anamsifia Raila Odinga kwa hatua ya kumchagua Martha Karua kama mgombea mwenza wa Azimio kwenye uchaguzi wa Agosti 9 ambapo alienda mbali zaidi na kusema kuwa Kenya ipo salama mikononi mwa Odinga na Karua.