Mwanamuziki nyota kutoka Marekani, Beyonce, ameteuliwa kuwania tuzo ya Emmy kwa vipindi vinavyoonyeshwa mchana yaani ‘Daytime Emmy’ kutokana na wimbo wa kutambulisha kipindi cha mama yake cha Facebook kiitwacho “Talks with Mama Tina”
Beyonce aliwaongoza wanawe Blue Ivy, Sir na Rumi katika kuimba wimbo huo jambo ambalo lilimgusa sana Bi. Tina Knowles-Lawson. Kipindi chake ni cha mazungumzo na wageni mbalimbali ambao huwa anawakaribisha na chakula.
Uteuzi wa Beyonce kuwania tuzo ya vipindi vya mchana kupitia wimbo huo wa kipindi cha mama yake ndio wa kwanza chini ya kitengo cha vipindi ambavyo huonyeshwa mchana lakini amewahi kuteuliwa mara nane kuwania tuzo ya Emmy kwa vipindi vinavyoonyeshwa usiku.
Kipindi cha Mama Beyonce kilianza rasmi Disemba mwaka jana na hadi kufikia sasa tayari amehoji wageni kadhaa wakiwemo Kelly Rowland, Zendaya, Chloe na Halle Bailey, Tiffany Haddish, Kevin Hart na Ciara.