Msanii mkongwe kwenye muziki nchini Uganda Catherine Kusasira amefunguka ya moyoni baada ya viongozi wa chama cha kisiasa nchini humo nrm kumtelekeza licha ya kutumia nguvu nyingi kuikinga kifua chama hicho kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2021.
Kupitia waraka mrefu aliouandika kupitia mtandao wake wa Facebook msanii huyo, amedai kwamba yeye pamoja na wasanii wenzake hawakuthaminiwa vya kutosha kwa kazi nzuri waliyowekeza katika chama cha NRM.
Kusasira amekiri hadharani kutoridhika na wandani wa chama cha NRM huku akifichua jinsi alivyopoteza marafiki, biashara, na mashabiki wakati akipigania chama hicho lakini cha kushangazwa mpaka sasa hajatuzwa kwa bidii yake.
Hata hivyo amesema watu walioelekezwa kuwazawadi wale waliowekeza nguvu zao na kujitolea kwa ajili ya chama cha nrm wamepora pesa zote huku wakiwaacha wakiandamwa na madeni.
Lakini pia Kusasira amemshauri rais Yoweri Kaguta Museveni kwamba watu anaowaamini watakuwa chanzo cha anguko lake.
Ikumbukwe Catherine Kusasira sio staa wa kwanza kuwachana viongozi wa NRM ambao wamekuwa na mazoea ya kujitakia makuu kwani kipindi cha nyuma tuliwaona mastaa kama Buchaman, Full Figure, na wengine wengi wakieleza malalamiko yao juu ya uongozi wa chama hicho.