Msanii wa muziki kutoka Kenya Dogo Richie ametangaza ujio wa EP yake mpya ambayo ni ya kwanza tangu aanze safari yake ya muziki.
Katika mahojiano na kipindi cha Interact Extra cha North Rift Radio Dogo Richie amesema Ep hiyo yenye jumla ya ngoma 8 za moto imekamilika kwa asilimia 100 na itaingia sokoni kabla ya ujio wa album yake mpya mwaka huu.
Licha ya kutoweka wazi jina na wasanii aliowashirikisha kwenye EP yake mpya, Dogo Richie amewataka mashabiki zake wakae mkao wa kula kuipokea EP yake hiyo ambayo kwa mujibu wake itakuwa na ladhaa ya kitofauti sana itakayokata kiu ya wafuasi wa muziki wake.
Utakumbuka Dogo Richie alipaswa kuachia album yake mpya mwaka 2020 lakini ilishindikana kutokana na janga la korona kusambaratisha baadhi ya mipango yake, jambo ambalo lilimpelekea kuahirisha mchakato mzima wa kuachia album hiyo.