Mwimbaji mkuu wa Sauti Sol Bien-Aime Baraza amempiga marufuku mchekeshaji Eric Omondi kuhudhuria tamasha lijalo la Sol Fest.
Katika taarifa aliyotoa kupitia ukurasa wake wa Instagram, Bien ameweka wazi kuwa Omondi hataruhusiwa katika ukumbi wa hafla hiyo kutokana na kitendo chake cha kuwazungumzia vibaya wasanii wa Kenya.
Hitmaker huyo wa “Inauma” ameongeza kuwa tayari wameagiza timu yao ya usalama kumzuia Omondi kuingia katika ukumbi wa tamasha lao la kila mwaka.
“Eric, mdomo wako mkubwa umekuponza! Usiwalaumu wanamuziki. Hakuna mtu anayetaka kukuona kwenye Sol Fest kwa hivyo tafadhali kaa mbali!!!”,
“Timu ya usalama ya Sol fest africa asubuhi ya leo imepokea maagizo makali ya kutoruhusu huyu jamaa na mbwa wake waliokopwa, karibu na ukumbi wa tamasha!..
“Binafsi, nimewasilisha zuio dhidi yake. Kwa hiyo, nawasihi nyote mumuepuke kama majanga!!!, Aliandika Instagram.
Hata hivyo, Eric Omondi alijibu kwa kusema kwamba anataka tiketi 20 za VIP na mbwa wake kupewa ulinzi maalum atakapohudhuria Sol Fest Disemba 9 mwaka huu.
Onyo hilo la Bien linajiri saa chache baada ya Omondi kusema kwamba atahitaji mbwa wasiopungua 20 ili aweze kuhudhuria Sol Fest kutokana na maisha yake kuwa hatarini.
Eric Omondi amekuwa akiwashambulia wasanii wa Kenya kila mara akisema kuwa wamezembea kwenye suala la kutoa nyimbo na kupelekea wasanii wageni kutawala tasnia ya muziki nchini.