Filamu maarufu ya ‘Black Panther: Wakanda Forever’ inayosubiriwa kwa hamu kubwa na wapenzi wa filamu Duniani kote iliyotayarishwa na Marvel Studio’s, inatarajiwa kuzinduliwa rasmi nchini Nigeria katika jiji la Lagos, kabla ya kutolewa kwake katika sinema ifikapo Novemba 11 mwaka huu.
Kwa mujibu wa taarifa, uzinduzi huu unatajwa kuwa ni wa Dunia nzima, na hayo yamebainishwa na Kampuni ya The Walt Disney wakishirikiana na Africa International Film Festival (AFRIFF) pamoja na FilmOne Entertainment.
Waanzilishi wenza wa FilmOne Entertainment, Moses Babatope na Kene Okwuosa, walielezea shauku yao kuhusu onyesho la kwanza na kutolewa kwa filamu hiyo, wakibainisha kuwa ni hatua muhimu kwa Afrika Magharibi. “Tunafuraha na tumejitolea kikamilifu kufanya kazi na Kampuni ya The Walt Disney kutoa onyesho la kwanza la Kiafrika.”