Mwimbaji Julius Owino almaarufu Juliani amekiri hadharani kuyumba kiuchumi baada ya walimwengu kumkejeli mtandaoni.
Katika video aliyochapisha kwenye instastory yake, Juliani amesema kuwa tatizo linalomkabili limechangiwa na hatua ya kutumia fedha zake kufadhili mipango yake bila wafadhili huku akifichua kuwa alichukua mikopo kwa ajili ya kukamilisha baadhi ya miradi.
Aidha amesema changamoto za kifedha anazokumbana nazo kwa sasa zimemfanya akose muda wa kukaa na mtoto wake huku akimshukuru mke wake Lilian Nganga kwa kumuelewa.
Katika hatua nyingine mwimbaji huyo amesema kuwa amejipa miaka 10 kutimiza ndoto aliyonayo kwa jamii yake ikiwemo kutengeneza ajira 10,000 na kutoa mikopo kwa wasanii.
Juliani, hata hivyo amebainisha kuwa licha ya kuyumba kiuchumi, bado ana uwezo wa kukidhi mahitaji yake ya msingi ambapo amewataka walimwengu kukoma kumfanyia mzaha mtandaoni kuhusiana na hali yake ya kiuchumi kwani inamuathiri kisaikolojia.