Rapa kutoka kenya Khaligraph Jones ameungana na Wakenya wengine kwenye mitandao ya kijamii kulaani kitendo cha wahudumu wa Boda Boda jijini Nairobi kumdhalilisha kijinsia mwanamke mmoja mara baada ya kudaiwa kumgonga kwa gari mhudumu mwenzao Machi 7 mwaka huu.
Kupitia ukurasa wake wa instagram Papa Jones ameonekana kutofurahishwa na kitendo cha wanabodaboda hao kumpakata mwanamke huyo hadi kumvua nguo ambapo amehapa kuwa mstari wa mbele kushinikiza vyombo vya usalama nchini iwape kifungo cha maisha waliohusika kutekeleza kitendo hicho cha kikatili.
Hata hivyo Mastaa mbali na watumiaji wengi wa mitandao ya kijamii wameonekana kumuunga mkono rapa huyo huku wakitaka maafisa wa polisi kuhakikisha waliohusika wote wanatiwa baroni na kufunguliwa mashtaka mahakamani
Kauli ya Khaligraph Jones imekuja mara baada ya idara ya usalama kutoa taarifa kuwa takriban washukiwa 16 waliomdhalalisha mwanamke huyo wamekamatwa huku msako ukiendelea kuwasaka washukiwa wengine waliotekeleza kitendo hicho.