Mwanamuziki kutoka Uganda King Micheal ameapa kufadhili mchakato wa kuandaa uchaguzi mwingine wa Chama cha Wanamuziki Uganda (UMA) baada ya uchaguzi wa chama hicho kuahirishwa ghafla juma lilopita.
King Michael ambaye anawakilishi wasanii wa dancehall katika chama cha UMA amesema kuwa watu walioandaa zoezi la upigaji kura kwa njia ya mtandao katika chama hicho walifeli kwenye majukumu yao.
“Sidhani kama uchaguzi wa mtandaoni utafanya kazi hapa Uganda. Nitaandaa uchaguzi mwingine kwa kuwa mimi pia ni kiongozi katika UMA,” alidai.
Msanii huyo amesema uchaguzi ambao atauandaa utafanyika kwa mfumo wa kawaida ambao utatoa nafasi kwa watu kupanga foleni kwenye vituo vya kupigia kura huku akiwasihi wanaounga mkono wazo lake kumtafuta ili waweze kuweka mikakati zaidi.
“Chaguzi zangu zitakuwa za watu kupanga foleni kwenye vituo vya kupigia kura. Ninawaalika wanaounga mkono wazo hilo kunifikia,” alimalizia.
Utakumbuka uchaguzi wa UMA ulifutwa siku ya jumatatu wiki iliyopita baada ya king Saha na wafuasi wake kudai mfumo wa upigaji kura ulidukuliwa na mchakato mzima wa uchaguzi ulikumbwa na dosari.