Msimamizi wa Masoko na Maendeleo ya Wasanii katika ukanda wa Afrika Mashariki chini ya Sony Music Entertainment, Seven Mosha amesema kuwa ameshaanza kuwasaini wasanii kadhaa na watakuwa wanawatoa orodha ya wasanii wapya kadiri muda unavyosonga.
Katika mahojiano yake hivi karibuni Seven amesema msanii wa kwanza kumtoa ni Ferre gola kutoka DR Congo ambaye Machi 25, mwaka 2022 aliachia albamu inayokwenda kwa jina la Dynastie yenye nyimbo 16.
“Albamu yake imefanya vizuri sana, imeshika namba sita Ufaransa upande wa iTunes, kwa kweli nimefurahi sana, kazi yangu ya kwanza kuwa na matokeo kiasi hicho, vile vile inafanya vizuri DR Congo maana ndio nyumbani, pia kuna Cameroon na Ivory Coast,” amesema.
Seven amesema yeye kama Msimamizi yupo kwenye nchi za DR Congo, Zambia, Tanzania, Kenya, Uganda, Ethiopia, Sudan Kusini, Rwanda na Burundi, huko kuna wasanii anaowatazama na sio Tanzania na Kenya tu kama ambavyo watu wanafikiri.
Aidha amesema alipoingia Sony kuna mambo mengi anasimamia pamoja na mafunzo, kwa hivyo hata muda wa kuwa mtandaoni kama hapo awali ni mchache hadi imefika wakati anaona awe na mtu kusimamia mitandao yake.
“Kuna mafunzo ya mwaka mzima ambayo tulikuwa tunachukua, kwa hiyo mafunzo ya kwanza kuelewa kampuni jinsi inavyofanya kazi, kuna vitengo vingi sana kwenye lebo kama hii ambayo ipo dunia nzima,” amesema.
Katika mafunzo hayo ni kujua jinsi mikataba ilivyo, kila mkataba unamaanisha nini, kisha mambo ya fedha, masoko, promosheni, uzalishaji, leseni na uchapishaji kazi, huku kila sekta ilikuwa na takribani miezi miwili ya mafunzo.
“Halafu jua nasimamia kitengo cha Afrika Mashariki, ni nafasi ya uongozi, hivyo nikaingia kwenye mafunzo ya uongozi ambapo kwa sasa nipo kwenye mwezi wa tatu. Maana kuna sera za kampuni kubwa kama hii, unatakiwa kuwa mwangalifu, usiwaingize kwenye matatizo, hivyo taratibu na miongozo lazima niijue,” amesema Seven.
Utakumbuka Desemba 15, 2020 ndipo Seven aliteuliwa kushika nafasi hiyo akiwa na uzoefu wa kuwasimamia wasanii kwa zaidi ya miaka 17 sasa.