You are currently viewing LEO KATIKA HISTORIA DESEMBA MOSI KILA MWAKA ULIMWENGU HUADHIMISHA SIKU YA UKIMWI DUNIANI

LEO KATIKA HISTORIA DESEMBA MOSI KILA MWAKA ULIMWENGU HUADHIMISHA SIKU YA UKIMWI DUNIANI

Siku kama ya leo Desemba mosi kila mwaka ulimwengu huadhimisha siku ya Ukimwi duniani, siku ambayo imetengwa na Umoja wa Mataifa kutafakari na kuwakumbuka wale wote waliopoteza maisha yao kutokana na ugonjwa huu.

Maadhimisho ya leo  ambayo ni ya 32 yamefanyika katika maeneo mbalimbali duniani na kuambatana na semina, mikutano na warsha mbalimbali zilizohimiza juu ya kuweko uelewa na ufahamu zaidi kuhusiana na maradhi ya Ukimwi.

Maadhimisho haya yamekuwa yakiadhimishwa tangu mwaka 1988, lengo kubwa likiwa ni kutoa elimu kuhusu namna ya kuepuka ugonjwa huu. Lakini pia Siku hii ya Ukimwi Duniani hutumiwa na wanaharakati na wakuu wa nchi kutoa elimu kuhusu namna ya kuzuia maambukizi ya virusi vya HIV na ugonjwa wa Ukimwi, kupiga vita unyanyapaa na kuhimiza watu kwenda kufanya vipimo ili kujua hali zao.

Shirika la Afya Duniani (WHO) limesema kuwa, watu milioni 37 duniani, wanaishi na virusi vya Ukimwi huku vijana wakiendelea kuwa hatarini zaidi kuambukizwa hasa barani Afrika.

Watu wengine Milioni 22 walioambukizwa, wanatumia dawa ya AVR ambayo imesaidia watu wengi sana kuendelea kuishi.

Woga, unyanyapaa na kupuuza ni mambo ambayo yanaendelea kuitesa dunia katika mapambano dhidi ya ugonjwa huo ambao umesababisha vifo vya mamilioni ya watu tangu miaka 1980.

Takwimu zinaonyesha kuwa, maambukizi mapya yanaathiri idadi kubwa ya vijana walio na umri wa kati ya miaka 15 hadi 25 na kwamba, kati ya vijana watano, watatu  kati yao ni wa kike.

Uchunguzi wa WHO umebaini kuwa, asilimia 71 ya maambukizi mapya yanatokea barani Afrika, hasa eneo la Afrika Mashariki na Kusini mwa bara hilo.

Hata hivyo Dunia imo katika kasi ya kuutokomeza ugonjwa huu wa Ukimwi. Ili kuutokomeza kabisa ugonjwa wa Ukimwi ifikapo mwaka 2030 kama sehemu ya malengo endelevu ya maendeleo kutahitajika kuharakishwa uwekezaji, nia thabiti na ubunifu.

Mtazamo wa kasi ya utokomezaji wa Ukimwi kama ulivyoanishwa na shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na ugonjwa huo UNAIDS, ni pamoja na uwekezaji, malengo kuelekea maeneo, jamii na mipango ambayo italeta mafanikio makubwa.

Elim Robert

Robert Elim is an Editor with high interest and knowledge in the entertainment space, an industry he has been actively part of since childhood. Leads to breaking stories are welcome at elimrobert@gmail.com & contact@urbanspice.co.ke