Mbunifu maarufu wa mavazi nchini Marekani, Virgil Abloh amefariki dunia Novemba 28 mwaka huu akiwa na umri wa miaka 41.
Kupitia Taarifa iliyotolewa kwenye ukurasa wake rasmi wa instagram imesema sababu za kifo chake ni ugonjwa wa saratani ambao alikuwa akipambana nao kwa miaka miwili.
Marehemu Virgil Abloh alikuwa Mkurugenzi wa Ubunifu wa kampuni ya Louis Vuitton kwa upande wa mavazi ya Kiume tangu mwaka 2018 lakini pia alikuwa CEO wa Off-White, kampuni yake ya mavazi ambayo aliianzisha mwaka 2012.
Akiwa na taaluma ya Usanifu, Abloh aliingia kwenye ulimwengu wa mitindo Kimataifa akiwa mfanyakazi wa muda katika kampuni ya Fendi mwaka 2009 akiwa na swahiba wake wa nguvu rapa Kanye West.
Mwaka 2018 alitajwa na Jarida la Time kama miongoni mwa watu 100 wenye ushawishi mkubwa duniani.