Mwanamuziki Nubian na rafiki yake mkubwa Bobi Wine hawajaweza kutumbuiza kwa takriban miaka mitatu kwa sababu zinazohusiana na siasa pamoja na usalama wa taifa la Uganda.
Kuna kipindi Nubian Li alikamatwa na kupelekwa kwenye magereza ya Kitalya kwa miezi kadhaa lakini alikuja akaachiliwa baada ya wasanii wenzake kupasa sauti aachiwe huru.
Baada ya kuachiwa uhuru, alifunga ndoa na mpenzi wake wa muda mrefu, Gloria Mutoni kwenye harusi ya kifahari iliyoibua maswali mengi miongoni mwa wadau wa muziki nchini Uganda.
Watumiaji wengi wa mitandao ya kijamii walimkosoa Nubian Li kwa kuandaa harusi kipindi cha janga la korona lilikuwa limeathiri tasnia ya muziki lakini hakutishika na jambo hilo. Baadhi ya wasanii kama Madrat & Chiko, pamoja na Kalifah Aganaga walitumia mitandao ya kijamii kumshambulia.
Sasa akijibu mashambulizi Nubian amewataja wasanii wanaomkosoa kwa hatua ya kufanya ndoa kwa njia ya harusi kama wanafiki. Lakini pia amelaani wasanii wanaoiomba serikali kufungua matamasha ya muziki kwa mara nyingine baada ya miaka miwili akisema kuwa aliposimamishwa na serikali kutumbuiza pamoja na Bobi Wine, wote walinyamaza.
Hata hivyo Nubian Li amewashauri wasanii kuchukua janga la korona kama somo na kujifunza kuzungumza kwa sauti moja pale panapotokea tatizo.