Mwanamuziki Moses Ssali maarufu Bebe Cool kwa mara nyingine tena amegonga vichwa vya habari kwa tuhuma za kuiba mdundo wa wimbo wake mpya uitwao ““Don’t Stop”.
Kulingana na mtayarishaji wa muziki aitwaye Bobix Pro ameumizwa na kitendo cha bosi huyo wa Gagamel kutumia kazi yake bila idhini.
Mtayarishaji huyo maarufu anadai Bebe Cool na watayarishaji wake, walitumia ubunifu wake wa kisanii katika wimbo wao mpya huku akidai alivunjika moyo alipotazama video hiyo na hakutajwa sehemu yeyote.
Bobix ameongeza kuwa hakutambuliwa na Bebe Cool kwani nembo yake iliyokuwa kwenye wimbo huo iliondolewa kwa njia ya kujaribu kuharibu ushahidi unaoonyesha wimbo huo ni wake.
Alipowasiliana na Bebe Cool kuelezea masikitiko yake kuhusu wimbo wake mpya kupitia GreenApp, Bebe Cool aliahidi tu kurekebisha makosa yake kupitia ukurasa wake wa Facebook atakapoanza rasmi kutangaza wimbo huo.
Mtayarishaji Bobix hakuridhishwa na maelezo ya Bebe Cool kwani alishangaa itamsaidia vipi kwani wimbo huo tayari umeanza kupigwa kwenye vituo tofauti vya redio na televisheni nchini Uganda.