Mwimbaji wa nyimbo za Injili ambaye pia ni mwaniaji wa kiti cha useneti kaunti ya Nairobi, Rufftone, amejitokeza na kuomba radhi kakake Daddy Owen na Wakenya kwa ujumla kutokana na kauli ya chuki aliyoitoa juzi kati dhidi ya kakake.
Rufftone amekiri kwamba alikuwa chini ya shinikizo na akaishia kumtumia kakake kueleza ni kwa nini alifikiri chama cha ODM kimekuwa kikihusishwa na uhuni.
Mwanasiasa huyo ametetea matamshi yake akisema alinukuliwa vibaya na watumiaji wa mitandao ambao walisambaza kauli yake hiyo.
Amesisitiza kuwa madai kuwa kakake alimtishia kwa panga yalilenga tu kuonyesha namna ambavyo Daddy Owen alivyokuwa na hasira wakati walitofautiana kimawazo mwaka 2007.
“Nilichomaanisha kumleta Daddy Owen ni kuwafanya Wakenya watambue kwamba siasa zinaweza kujipenyeza kati ya familia na ndiyo maana nikatumia mfano wa familia kwa sababu ndicho Wakenya wanaelewa zaidi, “Rufftone alisema.
“Samahani kwa nilichosema … nachukua jukumu kamili, ilikuwa bahati mbaya sana.
“Maoni niliyotoa yalikuwa jukwaa langu la kwanza la kisiasa katika runinga, kwa hivyo ninaomba Wakenya wanisamehe,” akaongeza.
Kwa upande wake msanii Daddy Owen pia amekiri kwamba alikuwa na shauku wakati wa uchaguzi wa mwaka 2007 lakini hajawahi kufanya vurugu.
“Nilipenda sana siasa 2007 na ODM iliposhindwa nilivunjika moyo sana lakini ninachojua ni kwamba sikuwahi kubeba panga na sijawahi kuwa na vurugu kwa sababu ya siasa. Nadhani kaka yangu alikuwa chini ya shinikizo wakati huo na ilibidi atoe mfano akitumia jina langu,” Daddy Owen alisema.