Hatimaye mwanamuziki Sheebah Karungi ameandikisha taarifa kwa polisi kuhusu kitendo cha kudhalalishwa kijinsia na mwanaume mmoja wiki kadhaa zilizopita.
Msemaji wa polisi nchini Uganda CP Fred Eranga amethibitisha habari hiyo kwa kusema Sheebah ametoa maelezo yote kuhusu mshukiwa aliyemdhulumu kingono kwenye moja ya onesho lake baada ya kuhojiwa na maafisa wa CID kwa muda, Mei 17 mwaka huu.
Eranga aidha amesema Sheebah amekanusha madai ya kunyanyaswa kimapenzi na mwanahabari tajika nchini Uganda Andrew Mwenda licha ya watu wengi kumshuku kuhusika na kitendo cha kumdhalilisha kingono kwenye gari lake kabla ya show yake.
Hata hivyo amemshukuru msaniii huyo kwa kushirikiana na vyombo vya usalama kwenye kesi yake hiyo huku akitoa hakikisho kuwa uchunguzi ukikamilika mshukiwa atachukuliwa hatua kali za kisheria iwe funzo kwa wanaume wanaowanyanyasa wanawake kijinsia katika jamiii.
Utakumbuka wiki iliyopita Sheebah aligonga vichwa vya habari baada ya kujitokeza na kulaani kitendo cha kunyanyaswa kijinsia na mwanaume mmoja ambaye alidai kuwa anaheshimika katika jamii.
Kisa hicho kilizua mjadala mzito miongoni mwa wadau wa muziki nchini Uganda ambapo wengi walimtaka Sheebah amfungulie kesi mshukiwa huku wengine wakimtaka amuanike hadharani jina la mwanaume huyo jambo ambalo sheebah hakufanya.