Msanii Stevo Simple Boy amewaomba radhi mashabiki zake baada ya kukosa kutumbuiza kwenye tamasha la So Fire Fiesta lilofanyika Nyali, Kaunti ya Mombasa.
Kupitia taarifa aliyotoa kupitia ukurasa wake wa Instagram amewalaumu waandaji wa tamasha hilo kwa kushindwa kumlipa pesa zake kabla ya kupanda jukwaani.
“Naomba msamaha kwanza kwa mashabiki wangu na kushukuru management yangu MIB Africa mumejaribu Kadri wa uwezo wenu na mnapigania Sana kuniona juu kila wakati..Tunajaribu Sana kama wasani ila wakenya wenzetu ndo wanatudhulumu”, Alisema.
Stevo ambaye alikuwa alipaswa kutumbuiza kwenye show hiyo ambaye Ruger wa Nigeria alikuwa msanii kinara amesema kitendo cha kususia kupanda jukwaani kulimpelekea kufungiwa hoteli aliyokuwa amekodishwa na waandaji wa So Fire Fiesta.
“Tulifungiwa hotelini kwa sababu tumekataa kuperfom bila kulipwa na kampuni ya sofire fiesta Ni tendo ambalo limenifika kooni kama Msanii na imenikataa moyo Sana ila sikati tamaa kabisa ntazidii kupambana na nawapenda sana wakenya wanao ni support.”, Aliongeza.
Hata hivyo mashabiki wamechukizwa na hatua ya waandaji wa So Fire Fiesta kutaka kumdhulumu Stevo Simple Boy huku wakionekana kumnyoshea kidole cha lawama mchekeshaji Eric Omondi kwa masaibu yaliyompata msanii huyo kwa kusema kuwa huenda alishirikiana na wasimamizi wa tamasha hilo kumfanyia mchezo mchafu.