Ndugu na watu wa karibu wa Mwanamuziki wa rap kutoka nchini Marekani Markelle Morrow maarufu kama Goonew aliyeuawa kwa kupigwa risasi huko District Height Maryland, Machi 28 Mwaka huu, Wameibua gumzo kubwa kote duniani baada ya kuupeleka mwili wa rapa huyo kwenye klabu ya usiku na kisha kuusimamisha mbele ya idadi kubwa ya watu kwa kile walichodai kuwa ni tukio maalum la kumuaga kwa kumpa heshima za mwisho na kusherehekea maisha ya rapa huyo.
Kinyume cha matarajio ya wengi, mwili wa rapa huyo uliingizwa katika klabu ya usiku ambapo muziki ulikuwa ukirindima huku kundi kubwa la watu waliohudhuria wakionesha kusherehekea wakiimba kwa furaha.
Maiti ya mwanamuziki huyo ilisimamishwa kwenye jukwaa ikiwa imeshikizwa kwenye ukuta ikiwa imevalia mavazi mithili ya mtu aliye hai.
Kufuatia tukio hilo la kustaajabisha maelfu ya watu wamekuwa na mitazamo tofauti juu ya tukio hilo, huku watu wa karibu wa rapa huyo wakidokeza kuwa suala hilo ni sehemu ya kutekeleza akichokiomba marehemu mwenyewe enzi za uhai wake kuwa afanyiwe hivyo atakapokuwa amekufa.
Kwa mujibu wa ripoti za TMZ inaelezwa kuwa bado uchunguzi unafanyika kubaini ukweli wa agizo hilo la marehemu.