Msanii wa Hip Hop Tanzania, Young Lunya amesema kusainiwa na Sony Music Africa ilikuwa ni kiu yake ya muda mrefu kwani lengo lake ni kufikisha muziki wake kimataifa na tayari alishajiandaa kwa hatua hiyo.
Young Lunya amesema ngoma zake nyingi alizorekodi zinalenga soko la kimataifa, hivyo alikuwa anahitaji Menejimenti yenye uzoefu katika eneo hilo, hivyo kuwa chini ya Sony Music ni mafanikio kwake.
“Nimeipokea kwa furaha kwa sababu ndoto zangu zilikuwa ni kuja kufanya kazi na lebo kubwa ndio maana hata kazi zangu ambazo nilikuwa nazirekodi nilikuwa sizitoi hadi nije kupata uongozi ambao unakuwa unaelewa sana masuala ya muziki, kwa hiyo kwenda Sony Music ni kitu kikubwa sana,” amesema Lunya.
Kwa mujibu wa taarifa kwa umma iliyotolewa na Sony Music Africa Juni 3, 2022, tayari Lunya yupo kwenye maandalizi ya albamu yake ya kwanza ambayo amewashirikisha Diamond Platnumz, Khaligraph Jones, Sho Madjozi na wengineo.
Huu ni usajili ya pili uliyoufanya Seven Mosha tangu alipoteuliwa kuwa Msimamizi wa Masoko na Maendeleo ya Wasanii Afrika Mashariki chini ya Sony Music Entertainment, msanii wa kwanza kumsaini ni Ferregola toka DR Congo ambaye ameshaachia albamu yake, Dynastie yenye nyimbo 16.
Wimbo wa kwanza kwa Young Lunya kuuachia chini ya Sony Music unaitwa ‘Vitu Vingi’ ambao amesema unazungumzia mahusiano ya kimapenzi. “Nimezungumzia kwamba kichwa kina vitu vingi ila haimaanishi kwamba sikupendi (mpenzi wake). Bado napambana kwa ajili yako, kwa hiyo ni wimbo wa kimapenzi lakini wa kitofauti kidogo”.